Sunday, February 27, 2011

FAMILIA YA HAYATI BABA WA TAIFA WAIBASHIRIA CHADEMA KUTAWALA NCHI - 2015


Butiama, Mara
27. 02. 2011 - on 12.15
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimebashiriwa kuibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 na hivyo kuweza kuongoza nchi kwa mara ya kwanza baada ya miaka 50 ya uhuru.

Ubashiri huo umetolewa jana kijijini Butiama na mmoja wa watoto wa hayati baba wa Taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Bw. Magige Kambarage alipokuwa akitoa shukrani zake kwa viongozi wa CHADEMA waliokuwa wamekwenda kijijini Butiama kudhuru kaburi la hayati baba wa Taifa na kumjulia hali mama Maria Nyerere.

Bw. Kambarage aliwapongeza viongozi wa CHADEMA kwa uamuzi wao wa kuendesha maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima lengo likiwa ni kuzungumzia mstakabali wa Taifa la Tanzania.

Alisema pamoja na kwamba wapo baadhi ya watu wanaogombana katika mambo ya kisiasa lakini watu hao wanasukumwa kufanya hivyo kutokana na ujinga unaowakabili.

“Kugombana ndani ya siasa ni ujinga tu ndiyo unaotusumbua, mimi nasema kitendo hiki cha maandamano mlichokifanya ni kitendo kizuri sana, pamoja na kwamba mimi ni mwanachama wa CCM, lakini nakupongezeni,”

“Hizi safari za kutembea kwa miguu na kushirikiana na wananchi ni kitu muhimu, eleweni kwamba mna dhamana kubwa hivi sasa mbele ya umma wa Tanzania, kwani ninyi ndiyo kambi kuu ya upinzani hapa nchini, fanyeni kazi msije mkapoteza dhamana mliyokabidhiwa na wananchi, umma umeishawakubali,”  alieleza Bw. Kambarage.

Alisema katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, watu wengi hawakujitokeza kupiga kura, lakini wapo zaidi ya milioni 20 wenye haki ya kupiga kura, ambapo aliwataka viongozi hao wa CHADEMA wafanye kazi kubwa ya kuwatafuta waliko ili ifikapo mwaka 2015 waweze kupiga kura.

“Mimi nasema hawa ambao hawakupiga kura wapo wengi sana, watafuteni waliko, 2010 CCM tulipata kura milioni tano za urais, lakini naamini mkiwatafuta hawa waliopotea, katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015 CHADEMA mtazoa zaidi ya kura milioni sita na CCM tutaambulia kura milioni nne, naamini hivyo,” alieleza Bw. Kambarage.

Alisema moja ya kazi wa vyama vya upinzani nchini ni kuwainua watanzania katika mambo ambayo serikali iliyoko madarakani imeshindwa kuwatekelezea na kwamba hivi sasa watanzania wameisha kikubali chama cha CHADEMA na ndiyo maana wanakiunga mkono badala ya CCM, “…..nakuombeeni mungu aibariki kazi yenu,” alisema.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe alimweleza mama Maria Nyerere kuwa lengo la ziara yao hiyo ni kumjulia hali yeye na familia yake, kudhuru kaburi la hayati baba wa Taifa  na kuomba dua katika kaburi lake ikiwa ni katika kuenzi heshima aliyokuwa nayo katika Taifa la Tanzania.

“Nachukua fursa hii kukushukuru kwa heshima kubwa uliyotupatia ya kukubali kuja kukujulia hali pamoja na kuzulu kaburi la hayati baba wa Taifa, tunasema hii ni heshima kubwa kwetu sisi CHADEMA wakati tukiwa katika mkoa wa Mara kuendesha maandamano ya amani na mikutano ya hadhara kuzungumzia mstakabali wa Taifa letu,”

“Tunaomba utuombee kwa mungu ili tuweze kufanya kazi zeru vizuri na ikibidi kutuunga mkono, basi utuunge katika lolote lile ambalo tutahitaji kuungwa mkono na wewe, lengo letu ni moja tu kuwatumikia watanzania ili waweze na wao kufaidi matunda ya uhuru wa nchi yetu,” alieleza Bw. Mbowe.

Kwa upande wake mama Maria Nyerere aliwashukuru viongozi hao wa CHADEMA  kwa uamuzi wa kumtembelea ili kumjulia hali ambapo aliwaombea kwa mungu aweze kuwapa afya njema na waendelee kuwatumikia wananchi kwa haki bila ya upendeleo wowote.

Msafara wa viongozi wa CHADEMA ukiongozwa na mwenyekiti wake wa Taifa, Bw. Freeman Mbowe na katibu mkuu wake Dkt. Wilbroad Slaa uliwasili kijijini Butiama saa 6.00 mchana jana na kupokelewa na mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mara Bw. Makongoro Nyerere ambaye ni mmoja wa watoto wa hayati baba wa taifa.

CHADEMA WATINGA BUTIAMA KWA HAYATI BABA WA TAIFA, MWALIMU JULIUS NYERERE

MAKONGORO NYERERE, AMBAYE NI MWENYEKITI WA CCM MKOA WA MARA AKIWA NA MWENYEKITI WA TAIFA YA CHADEMA, BW. FREEMAN MBOWE PAMOJA NA MAMA MARIA NYERERE WAKIELEKEA KATIKA KABURI LA HAYATI BABA WA TAIFA, MWALIMU NYERERE SIKU AMBAYO VIONGOZI WA CHADEMA TAIFA WALITEMBELEA KIJIJINI BUTIAMA, MKOANI MARA, FEBRUARI 27, 2011.
MWENYEKITI WA TAIFA WA CHADEMA, BW. FREEMAN MBOWE (Aliyeshika fimbo) NA MAMA MARIA NYERERE PAMOJA NA KATIBU MKUU WA CHADEMA TAIFA, DKT. WILBROAD SLAA WALIPOKWENDA KIJIJINI BUTIAMA KUMJULIA HALI MAMA MARIA NYERERE PAMOJA NA KUZULU KABURI LA HAYATI BABA WA TAIFA ILIKUWA NI FEBRUARI 27, 2011.

VIONGOZI WA CHADEMA WAKITOA HESHIMA KATIKA KABURI LA HAYATI MWALIMU NYERERE

VIONGOZI WA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) WAKITOA HESHIMA ZAO MBELE YA KABURI LA HAYATI BABA WA TAIFA, MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE, KUTOKA KULIA NI MWENYEKITI WA TAIFA, BW. FREEMAN MBOWE, MAMA MARIA NYERERE, DKT. WILBROAD SLAA, MEYA WA MANISPAA YA MUSOMA, BW. ALEX KASURURA, BW. MAGIGE KAMBARAGE WANANE KUTOKA KULIA NI MWENYEKITI WA CCM MKOA WA MARA, BW. MAKONGORO NYERERE, AMBAYE PIA NI MTOTO WA HAYATI MWALIMU NYERERE.

Friday, February 4, 2011

ZIMA MOTO WAKISAIDIANA NA GARI LA JWTZ - KIZUMBI KUZIMA MOTO

KIKOSI CHA ZIMAMOTO MANISPAA YA SHINYANGA, KIKISAIDIANA NA ASKARI WA JESHI LA WANANCHI WA TANZANIA (JWTZ) KIKOSI CHA KIZUMBI KUZIMA MOTO ULIOWAKA KATIKA KITUO CHA MAFUTA CHA HASS - ENEO LA IBINZAMATA MANISPAA YA SHINYANGA. (Picha na Suleiman Abeid)

TUKIO LA MOTO KATIKA KITUO CHA MAFUTA, KAMANDA WA POLISI WA MKOA WA SHINYANGA ENEO LA TUKIO

KAMANDA WA POLISI WA MKOA WA SHINYANGA, BW. DIWANI ATHUMANI AKIWA KATIKA ENEO LA TUKIO LA MOTO ULIOTEKETEZA KITUO CHA MAFUTA, HAPA ANATOA MAELEKEZO YA KUSAIDIA KUZIMWA KWA MOTO HUO.

MOTO WAUNGUZA KITUO CHA MAFUTA SHINYANGA

UMATI WA WANANCHI UKISHUHUDIA TUKIO LA MOTO KATIKA KITUO CHA MAFUTA CHA IBINZAMATA - MANISPAA YA SHINYANGA.

MATUKIO YA MOTO KITUO CHA MAFUTA - IBINZAMATA SHINYANGA

MOTO MKUBWA ULIOSABABISHWA NA HITILAFU YA MOTA YA KUHAMISHIA MAFUTA UKITEKETEZA KITUO CHA MAFUTA CHA HASS PETROLEUM - IBINZAMATA MANISPAA YA SHINYANGA.

TANESCO SHINYANGA YALALAMIKIWA KUHUSU MGAO WA UMEME


Shinyanga.
WAKATI Shirika la ugavi wa umeme nchini (TANESCO) likiongeza makali ya mgao wa umeme kwa wateja walioko katika gridi ya Taifa, wateja wa mjini Shinyanga wamelalamikia kitendo cha baadhi ya watumishi wa shirika hilo kugeuza suala la mgao kuwa mradi wa kujipatia fedha.
Hatua hiyo inatokana na shirika hilo kutokuzingatia ratiba ya mgao kama ambavyo ulivyotangazwa kupitia katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini baada ya kuelezwa kuwepo kwa matatizo katika mitambo ya kuzalisha umeme.
Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti jana mjini Shinyanga, wateja hao walidai pamoja na kuwepo kwa ratiba ya mgao wa umeme lakini watumishi wa TANESCO hawafuati ratiba hiyo kutokana na kuyapendelea baadhi ya maeneo ya watu wazito kifedha.
Wateja hao walisema utaratibu wa mgao unaonesha kuwa kila eneo litakuwa likizimiwa umeme kwa masaa 10 nyakati za mchana na masaa matano kwa usiku kwa kupishana siku, lakini utaratibu huo haufuatwi kutokana na baadhi ya maeneo wanakoishi wananchi wa kawaida kuzimiwa umeme kila siku nyakati za usiku.
Walisema kwa kawaida iwapo eneo moja linazimiwa umeme tangu saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni, siku inayofuata eneo hilo hilo hutakiwa kuzimiwa umeme kuanzia saa 12.00 jioni hadi saa 5.00 usiku.
“Sasa ajabu sisi watu wa maeneo ya viwandani kwa siku tatu mfululizo tumekuwa tukizimiwa umeme kuanzia saa 12.00 mpaka saa 5.00 usiku, lakini ajabu maeneo ya mjini kati na kwa watu wazito hawa kwa siku zote hizo wamekuwa wakipata umeme kutwa nzima bila ya kuzingatia ratiba ya mgao.
“Tumejaribu kuulizia tukaelezwa kuwa sisi kwa vile eneo letu lipo katika viwanda, eti wenye viwanda wameomba kuwa wanawashiwa umeme nyakati za mchana na uzimwe usiku, hili ni tatizo,”
“Vipi wathaminiwe wenye viwanda na wananchi wa kawaida tuwe gizani kila siku kwa sababu yao, ina maana waliopanga suala la mgao hawakufahamu kuwa kuna maeneo ya viwanda?” alihoji mmoja wa wateja waliolalamikia hali hiyo.
Aidha yapo madai kuwa baadhi ya mitaa ambayo hapo awali ilikuwa ikiingizwa katika mgao wa kawaida hivi sasa njia yao imebadilishwa na kuunganishwa katika njia ya hospitali na maeneo nyeti kama vile polisi na nyumba za ibada.
Maeneo hayo kwa kawaida hayapaswi kuwa na mgao kutokana na umuhimu wake na kuhitajika muda wote yawe na umeme, lakini kwa mswahili wa kawaida kuunganishwa katika njia hiyo ni wazi inaashiria kuwepo kwa mianya ya rushwa.
Hata hivyo kaimu meneja wa TANESCO mkoani Shinyanga, Bw. Sanibella Mahenge alikanusha madai ya kuwepo kwa mianya ya rushwa katika suala la mgao wa umeme ambapo alisema kuongezeka kwa makali ya mgao huo kunatokana na matatizo yaliyopo katika mitambo inayosambaza umeme nchini.
“Si kweli kwamba kuna upendeleo katika ugawaji wa umeme, hapana, juzi kulitokea tatizo kule eneo la Ndembezi, ilibidi tuzime umeme ili kurekebisha hitilafu iliyojitokeza, lakini kwa mchana huo eneo hilo halikuwa katika ratiba ya kuzimiwa, hivyo tukaona tuwashe viwandani na usiku tuzime na tuweze kuwawashia wala wa eneo hilo la Ndembezi,”
“Bahati mbaya sana siku ya Alhamisi, Februari 3, 2011 tukapokea maelekezo mapya ya mgao wa kitaifa, ikabidi tupange ratiba mpya, lakini ratiba hiyo pia ikawa inaangukia watu wa viwandani wazimiwe umeme usiku,”
“Na hata leo (Ijumaa) bado pia tutawazimia usiku wateja wetu wa eneo la viwandani, hii ni baada ya kuagizwa sasa mgao utakuwa ni wa kila siku badala ya ule wa kwanza, kwa wapo watakaokuwa wakizimiwa nyakati za asubuhi kwa masaa 10, na usiku masaa matano,” alieleza Bw. Mahenge.  END.