Monday, January 10, 2011

MTUHUMIWA AJIRUSHA KUTOKA NDANI YA GARI LA POLISI - APASUKA KICHWA NA KUFA

Shinyanga

MKAZI wa eneo la New Stand Manispaa ya Shinyanga aliyetambuliwa kwa jina la Bw. Haji Omari (30) amekufa papo hapo baada ya kuruka kutoka ndani ya gari la polisi alipokuwa akijaribu kutoroka asipelekwe katika kituo cha polisi.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo lililotokea juzi tarehe 9.01.2011 saa 1.10 usiku eneo la shule ya sekondari Uhuru mjini Shinyanga, Bw. Omari aliruka kutoka ndani ya gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser namba PT. 1805 ambapo alianguka chini na kupasuka kichwa chake.

Mashuhuda hao walisema Bw. Omari alikuwa amekamatwa na polisi baada ya kusababisha ajali mbili tofauti huko eneo la Kambarage Manispaa ya Shinyanga wakati akiendesha gari aina ya Toyota Chaser lenye namba za usajili T. 901 ANL mali ya baba yake Bw. Omari Magoma.

Walisema mbali ya kuyagonga magari hayo pia Bw. Omari ambaye inadaiwa alikuwa amelewa wakati akiendesha gari hilo alimgonga mfanyabiashara ya ndizi Bi. Doris Auko (60) mkazi wa Kambarage aliyekuwa amepanga ndizi zake kando ya barabara eneo la kanisa la A.I.C Kambarage Shinyanga.

Mmoja wa mashuhuda hao alisema mbali ya kumgonga muuza ndizi huyo pia gari hilo liligonga mikokoteni iliyokuwa imepangwa kando ya barabara hiyo ambapo Bi. Auko alizimia na kukimbizwa katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga kupatiwa matibabu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Diwani Athumani alithibitisha kutokea kwa kifo hicho ambapo alisema ajali ya kwanza ilitokea eneo la Japanes corner ambapo Bw. Omari aliligonga gari aina ya Toyota Chaser kutokana na mwendo mkali aliokuwa nao na hata hivyo hakuweza kusimama.

“Sasa baada ya kuligonga gari hilo la kwanza ambalo hata hivyo polisi hawakuweza kupata namba wala jina la dereva wake, huyu bwana aliendelea kuendesha gari lake kwa mwendo kwa kasi lakini alipofika eneo la kanisa la A.I.C Kambarage aliligonga gari lingine lenye namba T. 192 AAB Toyota Chaser,”

“Hili gari lilikuwa likiendeshwa na dereva Bw. Joseph Tasia (49) ambalo liliharibika vibaya, na pia alimgonga muuza ndizi aliyekuwa jirani ambaye alizimia na kukimbizwa hospitali, wananchi kwa ushirikiano na polisi waliokuwa doria walimkamata huyo dereva na kumpakia ndani ya gari walilokuwa nalo,” alieleza kamanda Athumani.

Alisema hata hivyo wakati gari hilo linaelekea katika kituo cha polisi dereva huyo akiwa amepakiwa nyuma pamoja na polisi watatu wawili wakiwa na silaha na mmoja aliyekuwa amemshikilia, ghafla lilipofika eneo la shule ya sekondari Uhuru alijaribu kumsukuma polisi aliyekuwa na silaha na yeye akajirusha nje.

Kamanda Athumani alisema polisi aliyekuwa na silaha alikamata bomba za kwenye gari kitu ambacho kilimsaidia asianguke lakini hata hivyo mtuhumiwa alijipigiza chini na kichwa chake kupasuka kwa nyuma upande wa kisogoni na kufa papo hapo.

Alisema hivi sasa polisi inaendelea na uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo lakini hata hivyo anasema uchunguzi wa awali unaonesha chanzo chake ni dereva huyo kuendesha gari akiwa amelewa ambapo amewataka madereva wote kuheshimu sheria za barabarani na kwamba wanapokuwa wamelewa wasiendesha gari.

Tuesday, January 4, 2011

MWENYEKITI WA KITONGOJI CHA IGUDIJO KAHAMA AUAWA KIKATILI

Kahama 
 
JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linaendesha msako mkali wa kuwasaka watu au mtu waliohusika na kifo cha mwenyekiti wa kitongoji cha Igudijo wilayani Kahama Bw. Enos Banyanda (65) aliyeuawa kikatili kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
 
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Hussein Kashindye alisema mbali ya wauaji hao kumuua kikatili mwenyekiti huyo wa kitongoji pia walimfunga kamba shingoni na kuuning’iniza mwili wake juu ya dali ndani ya jengo ambalo halijakamilika ujenzi wake ili watu waamini alikuwa amejinyonga.
 
Kamanda Kashindye alisema mwili wa Bw. Banyanda uligunduliwa juzi saa 9.00 alasiri na wanakijiji ukiwa ndani ya jengo lililokuwa jirani na makazi yake baada ya siku tatu tangu alipotoweka nyumbani kwake.
 
Alisema siku tatu kabla ya kubainika kuwa Bw. Banyanda alikuwa ameuawa aliondoka nyumbani kwake kwa lengo la kumsindikiza baba yake mzazi aliyekuwa akirejea nyumbani kwake na kwamba baada ya hapo hakuweza kurejea tena nyumbani.
 
Kamanda Kashindye alisema mara baada ya taarifa za kupatikana kwa mwili wa Bw. Banyanda kupatikana, polisi walikwenda katika eneo la tukio na kuukuta mwili wake ukiwa umefungwa kamba shingoni na kuning’inizwa juu ya dali, lakini hata hivyo polisi waliokota kofia yake iliyokuwa imetupwa jirani.
 
“Hii kofia ya marehemu ilipookotwa ilikutwa ikiwa na damu nyingi, hali hii ilisababisha polisi wauchunguze vyema mwili wa marehemu ukiwa unaning’inia pale juu, ndipo katika uchunguzi huo walibaini alikuwa amechomwa na kichwani na kitu chenye ncha kali na kusababisha kifo chake,"
 
"Hawa wauaji waliamua kumfunga kamba na kumning’iza juu ili kupoteza lengo wananchi waelewe kuwa alikuwa amejinyonga wakati sivyo, hata eneo jirani na alipokutwa amening'inizwa palikuwa na dalili za miburuzo hali iliyoonesha wazi kabla ya kufanyika kwa mauaji palitokea purukushani za hapa na pale,” alieleza Bw. Kashindye.
 
Alisema hivi sasa polisi inaendelea na uchunguzi juu ya kifo hicho pamoja na kuendesha msako mkali wa kuwasaka wahusika wa mauaji hayo na kwamba hakuna mtu anayeshikiliwa.
 
Katika tukio lingine mkazi wa kitongoji cha Magata kijiji cha Bugandika Manispaa ya Shinyanga, Bw. Emmanuel Mlima (36) amekufa baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani.
 
Kamanda Kashindye alisema tukio hilo lilitokea juzi huko katika kijiji cha Bugandika saa 2.00 asubuhi ambako wanakijiji waligundua mwili wa Bw. Mlima ukiwa unaning’inia juu ya mti akiwa amekufa baada ya kujinyonga.
 
Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa huenda Bw. Mlima alifikia uamuzi huo wa kujitoa uhai kutokana na ugomvi wa kifamilia kati yake na wazazi wake, na kwamba polisi inaendelea na uchunguzi zaidi ili kuweza kubaini chanzo halisi kilichosababisha mwananchi huyo kuchukua uamuzi huo.
 

Sunday, January 2, 2011

MWANAFUNZI AKAMATWA KWA KUMBAKA MWANAFUNZI MWENZAKE

Kahama,
Shinyanga

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Kishimba wilayani Kahama akituhumiwa kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa shule ya msingi anayesoma darasa la sita mwenye umri wa miaka 11.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Diwani Athumani alimtaja mwanafunzi anayeshikiliwa kwa kosa hilo la ubakaji kuwa ni Frank Stephano (16) mkazi wa mjini Kahama na kwamba tukio hilo lilitokea juzi saa 1.30 usiku.

Kamanda Athumani alisema mtuhumiwa huyo alifanya unyama huo baada ya kumvamia mwanafunzi huyo wa kike  (Jina na shule vimehifadhiwa) aliyekuwa katika matembezi ya kusherehekea mwaka mpya huko katika kitongoji cha Nyasubi mjini Kahama ambapo alianza kumbaka kwa nguvu.

Hata hivyo alisema mwanafunzi huyo aliweza kupiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa wapita njia ambao walifika na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa ambapo walimpeleka katika kituo cha polisi cha mjini Kahama.

“Tunamshikilia mtuhumiwa huyo na baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tukio hilo tutamfikisha mahakamani kujibu shitaka la ubakaji, tunawashukuru wananchi waliowezeshwa kukamatwa kwake na kumfikisha mikononi mwa vyombo vya dola pasipo kujichukulia sheria mkononi,” alieleza Bw. Athumani.

Katika tukio lingine, polisi wilayani Bukombe inamshikilia mkazi wa wilaya ya Chato mkoani Kagera kwa kosa la kupatikana na pikipiki inayohisiwa aliipata kwa njia za wizi.

Kamanda Athumani alimtaja mtuhumiwa anayeshikiliwa kuwa ni Bw. Elius Joseph (25) mkazi wa Chato ambaye alikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita saa saba usiku akiwa na pikipiki aina ya SANLG yenye namba za usajili T. 896 BCM.

Alisema polisi waliokuwa doria huko katika kijiji cha Runzewe walimkamata mtuhumiwa huyo ambapo alipotakiwa kutoa maelezo juu ya uhalali wa kumiliki pikipiki hiyo alishindwa kufanya hivyo na hivyo kukamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

Mwisho.